Ndoto imetimia, hatimaye naingia Chuo Kikuu!

Na Erick Shigongo
Chanzo: Facebook 



Nikiwa mtoto nilitamani sana kusoma hadi chuo kikuu lakini sababu ya umasikini na mazingira magumu hasa shule nilizosoma, sikufaulu mtihani wa darasa la saba, nikarudia darasa  la saba katika shule nyingine lakini bado sikufaulu, nilijiona mjinga!

 Nikajaribu kupitia njia ya 'vikozi' vidogo ili hatimaye niingie chuo kikuu lakini sikufanikiwa, nikaachana na ndoto hiyo na kuanza  ujasiriamali na kwa kutumia kipaji cha kuandika ambacho Mungu alinipa  lakini walimu wangu hawakukiona kwani  siku zote waliniita mbumbumbu sababu nilipata sifuri ya hesabu, maisha yangu yakabadilika kabisa.

Pamoja na hayo yote ndoto ya kusoma chuo kikuu bado haikuniacha hasa pale nilipotukanwa mara kwa mara mitandaoni pamoja na yote niliyoyafanya kwamba nilikuwa mbumbumbu, nikaamua kuanza tena kufukuzia ndoto yangu ya kusoma chuo kikuu na kupata shahada na baadaye Phd!

Haikuwa rahisi mtu kuruka kutoka darasa la saba hadi chuo kikuu! Huwa haitokei, njia ya kwenda chuo kikuu ni kupitia kidato cha sita ama kuwa na diploma, nilitaka kuvunja utaratibu huu.

Baadaye nikasikia juu ya utaratibu mpya uitwao Recognition of Prior Learning (RPL) ambao walifanya watu wenye uzoefu ama waliofanya mambo fulani katika jamii bila kuwa na elimu wapewe mtihani wa majaribio, wakifaulu huruhusiwa kujiunga na chuo kikuu.

Nikakusanya vitabu vyangu ambavyo nimekwishaandika na kuvipeleke Tume ya Vyuo Vikuu na kuomba niruhusiwe kufanya mtihani huo, nikaruhusiwa, mwaka jana nikafanya na kufeli, sikukata tamaa, mwaka huu nikafanya tena na kufaulu, hivyo   mwezi wa tisa ninaanza mwaka wa kwanza nikiwa na mwanangu Butogwa ambaye kamaliza kidato cha sita!

Nimeandika ushuhuda huu hapa ili kumtia moyo mtu yeyote aliyekata tamaa popote pale ulimwenguni au anayejidharau sababu ni darasa la saba au hana kitu fulani, INUKA  SONGA MBELE JIFUNZE KILA SIKU ELIMU HAINA MWISHO N A UKIYATUMIA UNAYOJIFUNZA MAISHA YAKO HAYATABAKI KAMA YALIVYO...

Related Posts

Ndoto imetimia, hatimaye naingia Chuo Kikuu!
4/ 5
Oleh